Blogger Widgets

Newdeal Africa

Thursday, December 8, 2011

Mr. Ebbo amefariki dunia!


Msanii maarufu nchini Tanzania wa muziki wa kizazi kipya Bongo Flava anayeitwa Abel Loshilaa Motika au kama anavyojulikana na wengi kwa jina lake la kimuziki Mr. Ebbo amefariki dunia.

Msanii huyo alifariki dunia siku ya Ijumaa ya tarehe 2/12/2011 hospitalini katika mji wa Usa River mkoani Arusha nchini Tanzania kutokana na kuugua ugonjwa wa Mapafu kwa muda mrefu .

Msanii huyo ambaye alipata umaarufu wake nchini Tanzania na Afrika ya Mashariki nzima kutokana na staili yake ya kipekee katika uimbaji kwa kutumia lafudhi ya kabila la kimasai.

Ubunifu wake huyo wa kutumia lafudhi ya lugha ya kimasai huku akichanganya na vichekesho mbalimbali vilivyojumuisha maisha halisi ya Mtanzania ilimfanya nyimbo zake zikubalike na wengi.

Pamoja na usanii, Mr. Ebbo alikuwa pia mtayarishaji wa muziki kupitia studio yake binafsi iliyoitwa Motika Records iliyokuwa na maskani yake mjini Tanga.

Mr. Ebbo atakumbwa zaidi kwa nyimbo zake nyingi zilizomletea umaarufu katika medani ya muziki ndani na nje ya Tanzania.

Baadhi ya nyimbo zake maarufu zilikubalika na wengi ni Mi Mmasai,Fahari YakoMambo MbofumbofuKamongoNjaaTom and Jerry naMbado.

Unaweza kuzisikiliza nyimbo zake hizo kwa kubonyeza linki za nyimbo hapo juu.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mount Meru mjini Arusha huku mipango ya mazishi ikiendelea kufanywa wakisubiri ndugu, jamaa na marafiki ambao wengine wako nje ya nchi.

Mr. Ebbo ameacha mke na watoto watatu na anatarajiwa kuzikwa katika mji wa Moshono mkoani Arusha.

Mungu Ailaze Roho ya Marehemu Mahala Pema Peponi.
BLOG HII IMEPOKEA TAARIFA ZA MSIBA WA MSANII  MR EBBO KWA MASIKITIKO MAKUBWA, TUNAUNGANA KWA PAMOJA NA FAMILIA YA MAREHEMU  NA  WATANZANIA POPOTE WALIPO KATIKA KUOMBOLEZA MSIBA HUU. MR EBBO ATAKUMBUKWA KWA UWEZO WAKE MKUBWA  WA KISANII NA KUELIMISHA JAMII KUPITIA SANAA YA MZIKI. RIP!

0 comments: