Blogger Widgets

Newdeal Africa

Sunday, May 8, 2011

DIASPORA CONFERENCE UK
Na Ally Kondo, London

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe (pichani) ameainisha baadhi ya changamoto anbazo Serikali inakabiliana nazo tangu ilivyoanza mchakato wa kuwahamasisha Watanzania wanaoishi ughaibuni (Diaspora) kushiriki katika kuchangia maendeleo ya nchi yao.
Waziri Membe alianisha changamoto hizo wakati akihutubia mkutano wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Uingireza tarehe 07 Mei, 2011. Waziri alieleza kuwa, moja ya changamoto hizo ni kujua idadi kamili ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi.
Katika kujaribu kutatua tatizo hilo, Membe alizielekeza Balozi na vyama vya watanzania wanaoishi ughaibuni kubuni mikakati itakayowezesha kupata idadi kamili ya watanzania wanaoishi nje. Waziri Membe aliagiza jukumu hilo litekelezwe katika kipindi cha mwaka mmoja.
Alieleza kuwa, sababu ya yeye kuja London kuhudhuria mkutano huo ni kukusanya hoja kutoka kwa wadau hao ili ziweze kusaidia suala la Diaspora kupelekwa Bungeni na hatimaye kuingia katika Katiba.
Waziri Membe alieleza kuwa, changamoto nyingine ni kwamba watu wengi hawafahamu vizuri maana ya Diaspora na kueleza kuwa, jitihada za makusudi zinahitajika kueleimisha umma kuhusu maana kamili ya neno Diaspora.
Akifafanua maana hiyo, Membe alieleza kuwa Diaspora ni walowezi wa Kitanzania wanaoishi nje ya nchi na kwamba bado wanajitambulisha kama Watanzania. Alisisitiza kuwa, wanafunzi wanaosoma nje ya nchi katika kipindi cha masomo yao iwe miaka miwili au mitatu hao sio Diaspora.
Waziri Membe pia aligusia suala la uraia pacha. Alieleza kuwa, nchi zinazoruhusu uraia pacha zimewafanya watu wao kupata kazi nzuri zenye mishahara mikubwa na hivyo kuwawezesha kutuma wanapotoka fedha nyingi.
Changamoto nyingine ambayo Waziri Membe aliitaja ni kubuni utaratibu bora wa kuwashirikisha Watanzania wanaoishi ughaibuni kuchangia maendeleo ya nchi yao. Alieleza kuwa, Serikali itaendelea kuzisawishi asasi mbalimbali kuhudhuria mikutano ya Diaspora. Kwenye mikutano hiyo asasi hizo zitafafanua fursa za kiuchumi zinazopatikana nyumbani ili jumuiya ya Diaspora ipime yenyewe kuendelea kukaa nje au kurudi nyumbani kutumia fursa hizo.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuwa na jarida la Diaspora litakalokuwa na taarifa zinazojiri nyumbani na nje ya nchi. Jarida hilo litasaidia kuwaunganisha watanzania walio nyumbani na wale wa nje ya nchi kuhusu taarifa mbalimbali zenye maslahi kwao.
Wajumbe waliohudhuria mkutano huo walipata fursa ya kutoa mawazo yao mbele ya Waziri. Mjumbe mmoja alipendekeza kuwe na kituo maalum cha kuratibu masuala ya Diaspora kama vile Kituo cha Uwekezaji kinavyoratibu masuala ya uwekezaji nchini Tanzania.
Aidha, mjumbe mwingine alishauri wakati wa Sensa inayotarajiwa kufanyika mwakani kubuniwe maswali ambayo yatawezesha kujua idadi ya watanzania wanaoishi nje ya nchi.
Wazo la kuanzisha kumbukumbu mkeka (database) ya ujuzi na fani walizonazo watanzania wanaoishi nje ya nchi lilitolewa. Kumbukumbu mkeka hiyo itumike wakati Serikali au asasi za kiraia kupata watu wanaowahitaji zinapotokea nafasi za kazi. Hii pia izingatie kuanisha kazi maalum kwa ajili ya jumuiya ya watanzania wanaoishi ughaibuni.
Mkutano wa Diaspora unafanyika kwa mara ya tatu nchini Uingereza ambapo mwaka huu wajumbe takriban 55 kutoka sekta ya umma na sekta binafsi wanahudhuria mkutano huo wakiwamo wabunge wawili pamoja na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi.

0 comments: